Mathayo 25:1-45 ONEN - Bible AI

1“Wakati huo, Ufalme wa Mbinguni utakuwa kama wanawali kumi waliochukua taa zao na kwenda kumlaki bwana arusi.*

2Watano wao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara.*

3Wale wapumbavu walichukua taa zao lakini hawakuchukua mafuta ya akiba,*

4lakini wale wenye busara walichukua taa zao na mafuta ya akiba kwenye vyombo.*

5Bwana arusi alipokawia kuja wale wanawali wote wakasinzia na kulala.*

6“Usiku wa manane pakawa na kelele: ‘Tazameni, huyu hapa bwana arusi! Tokeni nje mkamlaki!’*

7“Ndipo wale wanawali wote wakaamka na kuzitengeneza taa zao.*

8Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara, ‘Tupatieni mafuta yenu kidogo; taa zetu zinazimika.’*

9“Lakini wale wenye busara wakawajibu, ‘Sivyo, hayatutoshi sisi na ninyi pia. Afadhali mwende kwa wauzao mkajinunulie mafuta yenu.’*

10“Nao walipokuwa wakienda kununua mafuta, bwana arusi akafika. Wale wanawali waliokuwa tayari wakaingia ndani pamoja naye kwenye karamu ya arusi na mlango ukafungwa.*

11“Baadaye wale wanawali wengine nao wakaja, wakaita, ‘Bwana! Bwana! Tufungulie mlango!’*

12“Lakini yeye bwana arusi akawajibu, ‘Amin, amin nawaambia, siwajui ninyi!’*

13“Kwa hiyo kesheni, kwa sababu hamjui siku wala saa.*

14“Tena, Ufalme wa Mbinguni ni kama mtu aliyetaka kusafiri, naye akawaita watumishi wake na kuweka mali yake kwenye uangalizi wao.*

15Mmoja akampa talanta*+ 25:15 Talanta moja ilikuwa sawa na mshahara wa kibarua wa miaka 15.*tano, mwingine talanta mbili, na mwingine talanta moja. Kila mmoja alipewa kwa kadiri ya uwezo wake. Kisha yeye akasafiri.*

16Yule aliyepewa talanta tano akaenda mara moja akafanya nazo biashara akapata talanta nyingine tano zaidi.*

17Yule aliyepewa talanta mbili akafanya vivyo hivyo, akapata nyingine mbili zaidi.*

18Lakini yule mtumishi aliyekuwa amepokea talanta moja, alikwenda akachimba shimo ardhini na kuificha ile fedha ya bwana wake.*

19“Baada ya muda mrefu, yule bwana wa wale watumishi akarudi na kufanya hesabu nao.*

20Yule mtumishi aliyepokea talanta tano akaja, akaleta nyingine tano zaidi. Akasema, ‘Bwana uliweka kwenye uangalizi wangu talanta tano. Tazama, nimepata faida ya talanta tano zaidi.’*

21“Bwana wake akamwambia, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu! Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache; nami nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’*

22“Yule mwenye talanta mbili naye akaja. Akasema, ‘Bwana, uliweka kwenye uangalizi wangu talanta mbili. Tazama nimepata hapa talanta mbili zaidi.’*

23“Bwana wake akajibu, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache; nami nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’*

24“Kisha yule mtumishi aliyepokea talanta moja akaja, akasema, ‘Bwana, nilijua kwamba wewe ni mtu mgumu, unayevuna mahali usipopanda na kukusanya mahali usipotawanya mbegu.*

25Kwa hiyo niliogopa, nikaenda, nikaificha talanta yako ardhini. Tazama, hii hapa ile iliyo mali yako.’*

26“Bwana wake akajibu, ‘Wewe mtumishi mwovu na mvivu! Ulijua kwamba ninavuna mahali nisipopanda na kukusanya mahali nisipotawanya mbegu.*

27Vyema basi, ingekupasa kuweka fedha yangu kwa watoa riba, ili nirudipo, nichukue ile iliyo yangu na faida yake.*

28“ ‘Basi mnyangʼanyeni hiyo talanta, mkampe yule mwenye talanta kumi.*

29Kwa maana kila mtu aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyangʼanywa.*

30Nanyi mtupeni huyo mtumishi asiyefaa nje, kwenye giza, mahali ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.’*

31“Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi juu ya kiti cha enzi cha utukufu wake.*

32Mataifa yote watakusanyika mbele zake, naye atawatenga kama mchungaji anavyotenga kondoo na mbuzi.*

33Atawaweka kondoo upande wake wa kuume, na mbuzi upande wake wa kushoto.*

34“Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njooni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu; urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu.*

35Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha,*

36nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’*

37“Ndipo wale wenye haki watakapomjibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakulisha, au ukiwa na kiu tukakunywesha?*

38Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha, au ukiwa uchi tukakuvika?*

39Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza, au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’*

40“Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.’*

41“Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake.*

42Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha,*

43nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza, na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’*

44“Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’*

45“Naye atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’*

e>