1“Mimi ndimi mzabibu wa kweli na Baba yangu ndiye mkulima.*
2Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda, Baba yangu hulikata, nalo kila tawi lizaalo, hulisafisha ili lipate kuzaa matunda zaidi.*
3Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililonena nanyi.*
4Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda lisipokaa ndani ya mzabibu, vivyo hivyo ninyi msipokaa ndani yangu hamwezi kuzaa matunda.*
5“Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana, maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lolote.*
6Mtu yeyote asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi kama hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea.*
7Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo, nanyi mtatendewa.*
8Kwa hiyo Baba yangu hutukuzwa, kwa vile mzaavyo matunda mengi, nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.*
9“Kama vile Baba alivyonipenda mimi, hivyo ndivyo mimi nilivyowapenda ninyi. Basi kaeni katika pendo langu.*
10Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.*
11Nimewaambia mambo haya ili furaha yangu iwe ndani yenu na furaha yenu iwe kamili.*
12Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi.*
13Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.*
14Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru.*
15Siwaiti ninyi watumishi tena, kwa sababu watumishi hawajui bwana wao analofanya, bali nimewaita ninyi rafiki, kwa maana nimewajulisha mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu.*
16Si ninyi mlionichagua, bali mimi ndiye niliyewachagua ninyi na kuwaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kudumu. Ili nalo lolote mtakalomwomba Baba katika Jina langu, awape ninyi.*
17Amri yangu ndiyo hii: Mpendane.*
18“Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba ulinichukia mimi kabla yenu.*
19Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungeliwapenda kama vile unavyowapenda walio wake. Kwa sababu ninyi si wa ulimwengu, lakini mimi nimewachagua kutoka ulimwengu, hii ndiyo sababu ulimwengu unawachukia.*
20Kumbukeni lile neno nililowaambia, ‘Hakuna mtumishi aliye mkuu kuliko bwana wake.’ Kama wamenitesa mimi, nanyi pia watawatesa. Kama wamelishika neno langu, watalishika na neno lenu pia.*
21Watawatendea ninyi haya yote kwa ajili ya Jina langu, kwa sababu hawamjui yeye aliyenituma.*
22Kama sikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa hawana udhuru kwa ajili ya dhambi zao.*
23Yeyote anayenichukia mimi, anamchukia pia na Baba yangu.*
24Kama sikuwa nimefanya miujiza ambayo haijapata kufanywa na mtu mwingine yeyote, wasingalikuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa wameiona miujiza hii na bado wakatuchukia mimi na Baba yangu.*
25Lakini hii ni kutimiza lile neno lililoandikwa kwenye Sheria kwamba, ‘Walinichukia pasipo sababu.’*
26“Lakini atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, yaani, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi.*