1Mpeni Bwana, enyi mashujaa, mpeni Bwana utukufu na nguvu.
2Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake; mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake.
3Sauti ya Bwana iko juu ya maji; Mungu wa utukufu hupiga radi, Bwana hupiga radi juu ya maji makuu.
4Sauti ya Bwana ina nguvu; sauti ya Bwana ni tukufu.
5Sauti ya Bwana huvunja mierezi; Bwana huvunja vipande vipande mierezi ya Lebanoni.
6Hufanya Lebanoni irukaruke kama ndama, Sirioni+ 29:6 Yaani Mlima Hermoni. urukaruke kama mwana nyati.
7Sauti ya Bwana hupiga kwa miali ya umeme wa radi.
8Sauti ya Bwana hutikisa jangwa; Bwana hutikisa Jangwa la Kadeshi.
9Sauti ya Bwana huzalisha ayala, na huuacha msitu wazi. Hekaluni mwake wote wasema, “Utukufu!”
10Bwana huketi akiwa ametawazwa juu ya gharika; Bwana ametawazwa kuwa Mfalme milele.
11Bwana huwapa watu wake nguvu; Bwana huwabariki watu wake kwa kuwapa amani.